Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Mhe. Dkt. Mecktridis Mdaku, ameendelea na ziara ya mafunzo nchini China kwa kutembelea makumbusho na maeneo ya kihistoria na kiutamaduni, akijifunza namna nchi hiyo inavyohifadhi na kuenzi historia, mila na utamaduni wake.
Katika ziara hiyo, Mhe. Dkt. Mdaku ametembelea eneo la kihistoria na kiutamaduni la Old Street, ambako amejifunza kuhusu utamaduni wa majengo ya kale, historia ya Barabara ya Kale ya Hariri ya Baharini, utamaduni wa ufinyanzi wa Ni Xing Tao pamoja na tamaduni nyingine zilizohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Ziara hiyo imempa Dkt. Mdaku fursa ya kujionea namna China inavyotumia makumbusho kuhifadhi historia na utamaduni wake, huku ikihakikisha vizazi vipya vinaendelea kuifahamu na kuthamini historia ya waliowatangulia.
Akibeba somo hilo, amesema Tanzania pia ina utajiri mkubwa wa historia na urithi unaopaswa kutunzwa, kuendelezwa na kufikishwa kwa vizazi vijavyo.
“Nimeona namna wanavyothamini historia yao na kuhakikisha kizazi cha sasa kinaifahamu historia ya waliotangulia. Hili ni somo kwetu Tanzania kwamba tunapaswa pia kuendelea kuenzi na kutunza historia yetu.
Amesisitiza kwamba, watanzania tunapaswa kuwakumbuka watu waliopigania mila, utamaduni, ardhi na utu wa Watanzania, akiwemo Chief Mkwawa, na kuhakikisha vijana wetu wanaifahamu historia hiyo,” amesema Dkt. Mdaku.
Ameongeza kuwa, makumbusho hayapaswi kuonekana kama maeneo ya kuhifadhi vitu vya zamani pekee, bali ni vituo vya elimu, utamaduni na utalii vinavyoweza kujenga uzalendo na kuwasaidia vijana kuelewa walikotoka na thamani ya urithi wao.
Uzoefu huo umeendelea kumjengea Dkt. Mdaku mtazamo mpana kuhusu umuhimu wa kuhifadhi historia na urithi wa taifa, akieleza kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya maeneo ya kihistoria na kiutamaduni ambayo yakitunzwa vizuri yanaweza kuwa chanzo cha elimu, utalii na uzalendo kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Mbali na ziara hiyo ya kihistoria na kiutamaduni, Dkt. Mdaku ameshiriki katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la 9 la Kimataifa kuhusu Mito na Bahari (Estuaries) na Maeneo ya Pwani, ambako amepata fursa ya kujifunza kuhusu mazingira, mito na maeneo ya pwani.
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)