Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wilayani Nachingwea ametakiwa kukamilisha kazi hiyo mapema ili wananchi zaidi ya elfu 45 wanufaike na huduma hiyo.
Waziri wa Maji,Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemuagiza mkandarasi huyo Holtan Builders Ltd anayetekeleza mradi katika mji wa Nachingwea.
Mradi huo unaotekelezwa katika Kijiji cha Mkumba, una thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.5 na unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa maji hadi kufikia lita milioni moja kwa siku baada ya kukamilika. Hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa maji na kuboresha huduma kwa wakazi wa Mji wa Nachingwea.
Mhe. Aweso akizungumza na wananchi wakati akikagua mradi huo amesisitiza umuhimu wa wananchi kuanza kupata huduma ya maji safi na salama ambapo ameeleza Serikali inaendelea kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji inaondoshwa.
Mradi huo utanufaisha wakazi wa Nachingwea Mjini, maeneo ya Stesheni, Hospitali Camp, Majengo, California, Ugogoni, Mkumba Shamba na Nangoe.
