Ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuimarisha elimu bora na kuwawezesha waalimu, Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam kupitia mradi wake wa Gift of education, imedhamini semina ya kuwajengea waalimu wa shule za msingi za manispaa ya Kinondoni uwezo wa mbinu za mafunzo jumuishi.
Semina hiyo ya siku mbili iliyofanyika katika Shule ya Msingi Kinondoni hivi karibuni na kuhudhuriwa na walimu 84 kutoka shule za serikali katika manispaa hiyo iliandaliwa mahsusi ili kuwapa walimu mbinu za vitendo, ili kuongeza ushiriki wa darasani, kukuza mafunzo jumuishi, na kusaidia wanafunzi wenye mahitaji mbalimbali.
Semina hiyo ilihusisha mihadhara shirikishi, mijadala ya vikundi na mafunzo kwa vitendo yaliyotolewa na wataalamu wa udhibiti ubora wa manispaa ya KinondoniAkizungumza katika kilele cha mafunzo hayo, Ofisa Elimu wa Manispaa ya Kinondoni anayeshughulikia elimu ya msingi Deograsia Mapunda alisema semina hiyo imekuja wakati muafaka kwani ni kweli walimu wanahitaji kupigwa msasa kuhusu mbinu za mafunzo jumuishi.
Afisa Elimu huyo amesema kuwa mafunzo hayo muhimu yamewajengea waalimu uwezo utakaowewezesha kuwafikishia walimu taakriban 2,000 na wanafunzi wapatao 100,000 katika Manispaa ya Kinondoni, na hivyo kukuza ubora wa utolewaji wa elimu shirikishi kwa wanafunzi.
Aliipongeza Rotary Club ya Dar es Salaam kwa msaada huo mkubwa na kuahidi kuwa serikali itashirikiana bega kwa bega na Rotary katika mradi huu.Rais wa Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam, Abdulkadir Hameed alisema klabu hiyo inaelewa kuwa elimu ya kisasa inawahitaji walimu kutumia mikakati shirikishi ya kimaelekezo ambayo inawahusu wanafunzi mbalimbali, hivyo kuamua kuunga mkono katika kuwajengea uwezo walimu.
Tunaelewa kuwa ufundishaji shirikishi unahakikisha kwamba wanafunzi wenye mahitaji tofauti kama vile uwezo tofauti, ulemavu, mahitaji maalum na kadhalika wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kujifunza na tunaamini kuwa semina hii imewapa walimu ujuzi unaohitajika sana katika eneo hili.
Tunamshukuru afisa elimu wa Manispaa kwa ushirikiano wake mkubwa katika kufanikisha mafunzo haya. Pia tunawashukuru washiriki wote kwa mahudhurio makubwa na ni matumaini yetu kwamba watahamisha ujuzi huu muhimu kwa wenzao, alisisitiza rais huyo.
