Hati hiyo imesainiwa leo, Septemba 4, 2026, jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, pamoja na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Van Mo, Fathi Ahmed.
Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha mafunzo ya ufundi stadi yanaendana na mahitaji ya sekta ya viwanda na biashara, huku wahitimu wakijengewa umahiri, ubunifu, tija, maadili na uelewa wa usalama kazini, Van Mo pia itatoa fursa za mafunzo kwa vitendo na ajira kwa wahitimu wenye sifa zinazokidhi mahitaji yake.
Maeneo yatakayohusika katika makubaliano hayo ni pamoja na udereva wa magari makubwa, usimamizi wa vyombo vya usafiri, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo, usimamizi wa mnyororo wa ugavi, ukaguzi na ukarabati wa magari pamoja na mifumo ya umeme na elektroniki ya magari.
Maeneo mengine ni uendeshaji wa maghala na usimamizi wa stoo, uendeshaji wa vituo vya mafuta, ujenzi na usimamizi wa majengo na miundombinu, shughuli za utalii na ukarimu, pamoja na kilimo na uhifadhi wa mazao.
Katika mashauriano ya awali yaliyofanyika Agosti 31, 2026, Mkuu wa Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu wa Van Mo, Hamis Lugusha, alisema kampuni hiyo ina mahitaji makubwa ya madereva kutokana na ongezeko la magari, akieleza kuwa mwaka huu imepokea magari mapya 100 yanayohitaji madereva, huku magari mengine 150 yakitarajiwa kuongezwa mwakani.
Lugusha alisema pamoja na mahitaji hayo, kampuni imekuwa ikipata changamoto ya kupata madereva wanaokidhi viwango vinavyohitajika, hasa katika uadilifu, uaminifu, uwajibikaji na utamaduni wa kazi, hali hiyo imeifanya kampuni kuona umuhimu wa kushirikiana na VETA katika kuwaandaa madereva kuanzia misingi ya taaluma na maadili.
Kwa upande wake, CPA Kasore alisema programu hiyo inaweza kuwahusisha waombaji wenye mafunzo na wasio na mafunzo ya udereva, huku wenye uzoefu wakitakiwa kuchujwa kwa kuzingatia historia ya utendaji wao, alisema hatua hiyo itasaidia kupata waombaji ambao uzoefu wao unaendana na tabia na viwango vinavyohitajika na mwajiri.
Naye Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Abdallah Ngodu, alipendekeza ushirikiano huo utekelezwe kupitia mfumo wa uanagenzi, utakaowezesha Van Mo kushiriki katika kuwajenga wanafunzi kupitia mazingira halisi ya kazi, pamoja na kuwapa misingi ya nidhamu, uwajibikaji na utamaduni unaohitajika katika sekta ya usafirishaji.
Katika utekelezaji wa hati hiyo, VETA itatoa au kuwezesha programu za mafunzo, kushiriki katika uandaaji na mapitio ya mitaala, tathmini na utoaji wa vyeti vya umahiri, wakati Van Mo itatoa taarifa kuhusu mahitaji ya ujuzi, fursa za mafunzo kazini, mrejesho wa utendaji wa wanafunzi na wahitimu, pamoja na ajira kwa watakaokidhi vigezo vya kampuni.
.jpeg)


.jpeg)
