WAZIRI MKUU AISIFU TADB KWA KUCHOCHEA MAPINDUZI YA KILIMO




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Waziri Mkuu ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa mchango wake katika kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini, huku akiitaka kuongeza uwezo wa kifedha ili kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuharakisha mageuzi ya uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema uwekezaji wa benki hiyo umeendelea kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuinua kipato cha wananchi kupitia upatikanaji wa mitaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi.

Amesema Serikali inahitaji kuona TADB ikijengewa uwezo mkubwa zaidi wa kifedha ili iwe chanzo cha uhakika cha mitaji kwa sekta ya kilimo, akibainisha kuwa utegemezi wa ruzuku pekee hauwezi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakulima nchini.

"Wakulima wanahitaji taasisi imara ya fedha itakayowawezesha kupata mikopo ya kununua mbolea, pembejeo na kuwekeza katika uzalishaji. Ruzuku ina nafasi yake, lakini ina ukomo, hivyo lazima tujenge mfumo endelevu wa upatikanaji wa mitaji," amesema.

Aidha, ameitaka TADB kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na TAMISEMI kuwekeza katika ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao ili kuboresha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, hatua itakayowawezesha wakulima kuhifadhi mazao yao, kuyatumia kama dhamana ya mikopo na kuuza wakati bei zinapokuwa nzuri.

Amesema maboresho hayo yataongeza tija katika biashara ya mazao, kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna na kuongeza thamani ya uzalishaji wa wakulima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kufadhili miradi ya kimkakati inayobadilisha sekta ya kilimo nchini, ikiwemo umwagiliaji, mazao ya biashara na miradi ya kuongeza thamani ya mazao.

Amesema Serikali ya awamu ya sita imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mazingira wezeshi yaliyoifanya benki hiyo kukua na kuwafikia Watanzania wengi zaidi, huku akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mtaji wa benki hiyo.

Amesema TADB imeongeza uwezo wake wa kifedha kutoka Sh60 bilioni hadi Sh452.16 bilioni, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kuchochea ukuaji wa minyororo ya thamani ya kilimo nchini.

Amesema ongezeko hilo la mtaji limechangiwa na uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na ushirikiano na taasisi mbalimbali za maendeleo, hatua ambayo imeiwezesha kupanua huduma za kifedha na kuongeza uwezo wa kufadhili shughuli za uzalishaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

"Kabla ya uwekezaji wa Serikali , mtaji wa TADB ulikuwa Sh60 bilioni, lakini mwaka 2021 Serikali iliongeza Sh208 bilioni na kufanya mtaji kufikia Sh268 bilioni,mwaka 2024 mtaji huo uliongezeka kwa Sh174.16 bilioni kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), huku mwaka 2025 Serikali ikiongeza Sh10 bilioni na kufanya mtaji wa benki kufikia Sh452.16 bilioni,"amefafanua.


Mbali na mtaji wa Serikali, Mkurugenzi huyo amesema TADB imefanikiwa kuvutia rasilimali nyingine zikiwemo mikopo yenye thamani ya Sh445.6 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo, Mfuko wa Dhamana (SCGS) wenye thamani ya Sh108.4 bilioni pamoja na fedha za Sh36.54 bilioni zinazosimamiwa kwa niaba ya Serikali.

Amesema mafanikio hayo yameongeza uwezo wa benki kufadhili miradi ya kilimo, huku takwimu zikionyesha kuwa asilimia 73.6 ya mikopo yote ya benki imetolewa kati ya mwaka 2022 na 2025, kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, TADB itaendelea kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kimkakati, kukuza matumizi ya teknolojia katika uzalishaji pamoja na kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika biashara za kilimo.

"Zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetolewa kufadhili miradi ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini, huku vyama vya ushirika vinavyozalisha kahawa, hususan katika mikoa ya Kagera na Kigoma, vikiwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo,"amesema.

Nyabundege amesema TADB pia imewezesha mradi wa kisasa wa uzalishaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo, unaotumia teknolojia ya kisasa iliyopatikana kutoka Misri, ambayo kwa sasa ina uwezo wa kuhifadhi hadi tani 90 za samaki kwa mwezi kwa kuzingatia viwango vya utunzaji wa mazingira.

Amesema mradi huo umefungua soko kubwa la samaki, umeongeza thamani ya mazao ya uvuvi na umeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kwanza katika ukanda kutumia teknolojia hiyo ya kisasa katika sekta ya uvuvi.

Naye mnufaika wa mradi wa samaki wa Bagamoyo Bi.Farida amesema ufadhili wa TADB umewezesha matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kuhifadhi samaki, hatua iliyoongeza uzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao na kufungua masoko mapya ya ndani na nje ya nchi.

Amesema uwezo wa kuhifadhi tani 90 za samaki kwa mwezi umeongeza mapato ya biashara, umezalisha ajira kwa vijana na kuchangia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, hivyo kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza bidhaa zinazoweza kuzalishwa nchini.










Post a Comment