Na Baraka Messa – MAELEZO
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimesema kinaendelea kupanua wigo wa mafunzo kwa kuanza kuzalisha wataalam wa kada mbalimbali katika sekta ya usafirishaji na miundombinu ikiwemo ya SGR na usafiri majini hatua inayolenga kukidhi mahitaji na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika miradi ya kimkakati nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26, Agosti 3, jijini Dodoma Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Dkt. Prosper Mgaya, amesema awali NIT kilijikita zaidi katika kuzalisha madereva wa usafiri wa barabarani, lakini sasa kimebadilika na kuwa taasisi inayotoa wataalam wa nyanja mbalimbali za usafirishaji.
Amesema uwekezaji uliofanywa na Serikali katika miundombinu ya kisasa, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), umewezesha chuo kuanzisha programu za diploma na shahada ya kwanza zinazolenga kuzalisha wataalam watakaohudumia sekta hiyo muhimu ya uchumi.
“Awali NIT ilijikita zaidi kutoa wataalam wa udereva, lakini leo tunatoa wataalam wa sekta mbalimbali za usafirishaji na miundombinu ili kukidhi mahitaji ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali,” amesema Dkt. Mgaya.
Amesema NIT pia imepanua mafunzo katika sekta ya usafiri wa majini kwa kuanzisha kozi za diploma na shahada ya kwanza, sambamba na fani maalumu za ufundi wa utengenezaji wa meli na usanifu wa meli ambazo hapo awali zilikuwa hazipatikani nchini.
Dkt. Mgaya, amesema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kuwa na wataalam wa ndani wenye uwezo wa kubuni, kutengeneza na kuhudumia vyombo vya usafiri wa majini badala ya kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi.
Aidha, amesema chuo kinaendelea kuimarisha elimu ya ngazi za juu kwa kutoa programu nne za uzamili (Masters) katika eneo la usafiri wa majini, zenye lengo la kuzalisha mameneja na viongozi wenye uwezo wa kusimamia sekta ya usafirishaji kwa ufanisi.
Amesema maboresho hayo yanaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akieleza kuwa sekta ya usafirishaji ni uti wa mgongo wa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa, hivyo uwekezaji katika rasilimali watu ni nguzo muhimu ya kufanikisha malengo hayo.