DKT. MWINYI: USHIRIKIANO WA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI NI NGUZO YANGUZO YA KUFANIKISHA DIRA YA TAIFA 2050

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akikabidhiwa nyenzo ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika hafla ya mkutano wa mazungumzo maalum kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, iliyofanyika leo Ikulu Dar es Salam, tarehe 3 Agosti, 2026.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameshiriki mkutano wa mazungumzo maalum kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Mkutano huo umefanyika leo Ikulu Dar es Salam, tarehe 3 Agosti, 2026.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na Sekta Binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kujenga Tanzania yenye uchumi shindani, jumuishi na unaojitegemea.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 3 Agosti 2026, aliposhiriki Mkutano wa Mazungumzo Maalum kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi na msukumo anaoutoa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inaweka mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania na ustawi wa wananchi kuelekea mwaka 2050.

Aidha, amesema Dira hiyo inaweka msingi wa kujenga uchumi unaozingatia tija, ubunifu, matumizi ya teknolojia na ushiriki mkubwa wa Sekta Binafsi. Amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika viwanda, biashara, utalii, uchumi wa buluu, kilimo cha kisasa, huduma za kifedha, uchumi wa kidijitali pamoja na maendeleo ya rasilimali watu.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha maeneo ya kimkakati yanapewa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Ameihimiza Sekta Binafsi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali kwa kuongeza uwekezaji katika maeneo ya kimkakati, kutumia teknolojia za kisasa, kuongeza tija na kuimarisha ubia utakaochangia kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya muda mrefu ya Taifa.

Akihitimisha salamu zake, Rais Dkt. Mwinyi amesema ana imani kuwa mkutano huo utaimarisha zaidi ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi na kuongeza msukumo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa manufaa ya Watanzania wote.

Sambamba na hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kushuhudia utiaji saini wa matamko ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika utekelezaji wake.

Matamko hayo yanaonesha dhamira ya pamoja ya kuongeza uwekezaji, kuendeleza ubunifu, kukuza uzalishaji wenye tija na kuimarisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050.

Miongoni mwa waliosaini matamko hayo ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo, kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wafanyabiashara, Wawekezaji, Mabalozi, Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa, Viongozi wa Dini, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na wageni waalikwa.

Post a Comment