MBUNGE LUTEVELE WA MAFINGA MJINI AIOMBA SERIKALI KUHARAKISHA UJENZI WA BARABARA YA MAFINGA–MGOLOLO

NA DENIS MLOWE, MUFINDI
MBUNGE wa Jimbo la Mafinga Mjini, Dickson Lutevele, ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara ya Mafinga–Mgololo  akisema ni kiungo muhimu cha uchumi wa Wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.Lutevele alisema licha ya barabara hiyo kuonekana kupitika wakati wa kiangazi, kipindi cha masika hali huwa ngumu na kuathiri usafirishaji wa mazao, mbao na bidhaa nyingine zinazochangia uchumi wa eneo hilo.

Akizungumza mbele ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, Lutevele alisema wananchi wa Mafinga Mjini wanategemea kwa kiasi kikubwa shughuli za uzalishaji zinazofanyika maeneo ya vijijini, hivyo kuboreshwa kwa miundombinu hiyo kutaimarisha biashara na kuongeza fursa za kiuchumi.

Alisisitiza kuwa wabunge wa Mkoa wa Iringa wamekuwa wakizungumza kwa pamoja kuhusu umuhimu wa mradi huo bungeni na kuomba Serikali ianze utekelezaji wake bila kuchelewa.

Akijibu ombi hilo, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtuma kuwasalimu wananchi wa Iringa na kusisitiza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa mkoa huo katika uzalishaji wa chakula, mazao ya misitu na vifaa vya ujenzi vinavyohudumia soko la ndani na nje ya nchi.

Ulega alisema Serikali tayari imekamilisha hatua muhimu za maandalizi ya mradi huo ambapo mkandarasi amepatikana na kilichobaki ni kutoa fedha za awali (advance payment) ili aanze kazi.

Alisema baada ya kutembelea eneo hilo amejionea umuhimu wa barabara hiyo katika kukuza uchumi wa Mufindi na Mkoa wa Iringa, hivyo atausimamia kwa karibu utekelezaji wake.

Alieleza kuwa amewapongeza wabunge wa Iringa kwa umoja wao katika kuwasilisha hoja kuhusu barabara hiyo, akisema wamekuwa wakitumia kila fursa ndani na nje ya Bunge kuishawishi Serikali kuipa kipaumbele.

Alisema kuwa juhudi hizo zimechangia yeye kufika eneo la mradi na kujionea hali halisi.
Waziri huyo alisema Serikali inalenga kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakwenda sambamba na uwekezaji mwingine ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani ili kuruhusu shughuli za biashara kufanyika saa ishirini na nne na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Mbali na barabara hiyo, Ulega alikagua jengo la wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.

Alisema fedha za kukamilisha mradi huo zipo na akawataka watendaji kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi, hususan wajawazito, waanze kupata huduma bora karibu na makazi yao.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dokta Linda Selekwa, alisema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu wilayani humo kupitia ujenzi wa shule mpya za msingi, awali na sekondari. 

Alieleza kuwa katika eneo la Mtwango, Serikali imetoa shilingi milioni 329 kujenga madarasa sita ya shule ya msingi na madarasa mawili ya elimu ya awali, huku mradi wa shule ya sekondari uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 500 ukiwa tayari umekamilika na kuanza kutoa huduma.

Dokta. Selekwa alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za elimu na maendeleo ya wananchi, huku Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ikiendelea kuchangia fedha za mapato ya ndani ili kuunga mkono juhudi hizo.

Post a Comment