Wakiwa katika banda hilo, maafisa hao walipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ikiwemo ushauri na miongozo kwa wananchi na wawekezaji kuhusu upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji na huduma za ardhi, fursa za biashara katika sekta za kimkakati zinazokuwa kwa kasi pamoja na taratibu za uwekezaji ndani ya jiji
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mkuu wa Divisheni ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Lusajo Mwasongwe alisema kuwa wamejifunza mambo mbalimbali yanayoweza kuwasaidia kuboresha utoaji wa huduma katika mamlaka zao. “Tumepata uzoefu mzuri katika banda hili kuhusu namna Jiji la Dodoma linavyotangaza fursa za uwekezaji na kutoa huduma kwa wananchi” alisema Mwasongwe.
Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ruth Kingu alisema kuwa maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuitangaza halmashauri na kuvutia wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali. “Tunawakaribisha wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kutembelea banda letu ili kupata huduma na kufahamu fursa mbalimbali zilizopo ndani ya Jiji la Dodoma" alisema Kingu.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaendelea kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara kwa lengo la kutangaza huduma zake, kuonesha fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo.
