WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGIA BILIONI 25 KUJENGA KITUO CHA MOYO KCMC

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) Profesa Gileard Masenga akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 9, 2026 jijini Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto kutoka KCMC Dkt. Ronald Mbwasi akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 9, 2026 jijini Dar es Salaam.

…………..

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) imetoa wito kwa Watanzania kushiriki katika uchangiaji wa ujenzi wa jengo la huduma za matibabu ya moyo. Kiasi cha shilingi bilioni 25 kinahitajika kukamilisha mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 9, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Profesa Gileard Masenga, amesema gharama za ujenzi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba na vifaa vya hospitali zinakadiriwa kufikia jumla ya shilingi bilioni 25.

Ameeleza kuwa wataalamu watakaohudumia kitengo hicho tayari wamepata mafunzo ndani na nje ya nchi, ikiwemo India, kwa ufadhili wa taasisi ya Global Heartcare Foundation.

Profesa Masenga amesema KCMC tayari imeingia makubaliano na wadau wa kimataifa waliokubali kugharamia asilimia 90 ya ujenzi huo. Hivyo, Watanzania wanahimizwa kuchangia asilimia 10 iliyobaki ili kufanikisha mradi huo.

Ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha ifikapo Julai 2027, huduma za matibabu ya moyo zinaanza kutolewa, hatua itakayosaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wengi nchini.

“Huu si mradi wa KCMC pekee, bali ni wa Watanzania wote. Unalenga kulinda maisha ya ndugu, wazazi, watoto na vizazi vijavyo,” amesema.

Amehimiza wananchi wa makundi yote, wakiwemo vijana, wazee, wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima, viongozi na Watanzania waishio diaspora, kuchangia kwa moyo wa uzalendo na mshikamano, akisisitiza kuwa kila mchango una thamani kubwa katika kuokoa maisha.

Kwa mujibu wake, michango inaweza kutolewa kupitia akaunti zifuatazo: Jina la akaunti: KCMC MOYO, Bank of Africa: 04563580007,  CRDB Bank: 0150686858800 ,  NMB Bank: 40310194610 , NBC Bank: 017172000770.

Mitandao ya simu: Mixx by Yas: 15175376 , Halotel (Halopesa): 23758475

Pia, wachangiaji wanaweza kufika moja kwa moja hospitalini kutoa misaada yao.

Profesa Masenga amesisitiza kuwa jukumu la kuboresha huduma za afya si la Serikali pekee, bali linahitaji ushirikiano wa wadau wote.

Amebainisha kuwa jengo hilo litakuwa la kisasa lenye ghorofa tatu, likijumuisha vyumba viwili vya upasuaji wa moyo, maabara mbili za uchunguzi wa mishipa ya moyo, vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) kwa watu wazima na watoto, vitengo vya uangalizi maalum baada ya ICU, vitanda 102 vya wagonjwa wa ndani, kliniki za nje, kitengo cha urekebishaji wa afya ya moyo pamoja na maabara na huduma za dawa.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto kutoka KCMC, Dkt. Ronald Mbwasi, amesema magonjwa yasiyoambukiza yanachangia takribani asilimia 70 ya vifo duniani, huku magonjwa ya moyo na mishipa yakiwa chanzo kikuu.

Amefafanua kuwa magonjwa kama kiharusi na kuziba kwa mishipa ya moyo yanachukua sehemu kubwa ya vifo hivyo, na zaidi ya asilimia 78 ya vifo hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Kwa mujibu wa takwimu za KCMC, asilimia 14.4 ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo ni wa magonjwa ya moyo, wakikaa kwa wastani wa siku 9 hadi 10. Aidha, asilimia 38.5 ya wagonjwa hurudi kulazwa tena baada ya kuruhusiwa, huku vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo vikifikia takribani asilimia 18.3 ya vifo vyote hospitalini hapo.

Post a Comment