Katibu mstaafu wa Chama cha watu wenye ulemavu wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Angelus Milinga,akizungumza jana kuhusu mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri za wilaya ambapo amewataka walemavu wenye kuhitaji mikopo hiyo kwenda kwenye Halmashauri zao kwa ajili ya kupata utaratibu wa mikopo hiyo.
Na Muhidin Amri,Songea
WATU wenye ulemavu mkoani Ruvuma,wametakiwa kuunda vikundi vitakavyowapa sifa ya kunufaika na uwezeshaji wenye lengo la kuwajengea uwezo wa kiuchumi na hatimaye kuondokana na umaskini.
Wameonywa juu ya tabia ya kukaa barabarani na kuzunguka kwenye maeneo ya starehe kwa ajili ya kuomba misaada badala yake wajitokeze kwenda Halmashauri kuchukua mikopo inayotolewa bila riba kutoka asilimia mbili ya mapato ya ndani ili waweze kujipatia kipato na kuondokana na umaskini.
Wito huo umetolewa jana na Mwanzilishi wa Chama cha walemavu wilayani Songea Angelus Milinga,wakati akizungumzia kuhusu mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri za wilaya kutoka kwenye mapato ya ndani.
“Naomba nitumie nafasi hii kuwaasa walemavu wenzangu,waache kukaa barabarani na kuomba misaada midogo midogo watu wamechoka kuwasaidia,waende Halmashauri kupata utaratibu wa mikopo inayotolewa na serikali tena bla riba,kuomba mara kwa mara ni fedhea kubwa kwa binadamu”alisema Milinga(Mateso).
Alisema,licha ya Halmashauri kufanya vizuri kwa kutenga fedha kwa mwaka hadi kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya watu wenye ulemavu lakini baadhi yao wamekuwa waoga kwenda kukopa fedha zinazotengwa kwa ajili yao.
“Natumia nafasi hii kuwasisitiza sana walemavu wenzangu watumie fursa iliyotolewa na serikali kwenda kukopa fedha ili wapate mitaji ya itakayowasaidia kufanya shughuli za kuwaingizia vipato,kila mwaka serikali kupitia Halmashauri zetu uwa inatenga fedha kwa ajili yetu”alisema Milinga.
Milinga,amewaasa watu wenye ulemavu wanaochukua mikopo hiyo kuhakikisha wana rejesha kwa wakati na kwa mujibu wa utaratibu uliopo ili kutoa fursa kwa kila mmoja anayehitaji kupata mikopo hiyo.
Milinga,ametoa wito kwa jamii kuwasaidia watu wenye ulemavu kufika kwenye ofisi za serikali za vijiji na Hamashauri za wilaya ili kupata utaratibu unaotumika kupata mikopo ya asilimia mbili ili waweze kuanzisha miradi itakayowaingizia vipato na hivyo kuondokana na umaskini.
Ameiomba jamii,kuacha kuwapa walemavu wanaokaa barabarani misaada kwani tabia hiyo imesababisha kuongezeko kwa idadi ya walemavu mitaani hasa maeneo ya mjini ambao wamekuwa kero kubwa.
“Serikali imetimiza wajibu wake kwa kupeleka fedha kwenye Halmashauri kwa ajili ya kuwasaidia walemavu,kwa hiyo sisi wenyewe ndiyo wenye jukumu na wajibu wa kuchangamkia fursa hiyo,mimi mwenyewe nimesaidiwa na Halmashauri kupata mikopo na sasa nashukuru namiliki biashara zangu za bajaji ambazo zinaniingizia kipato cha kula na familia yangu”alisema.
Mkazi wa Songea Njelela Mvula,ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga asilimia kumi kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya makundi maalum ya wanawake,vijana na wenye ulemavu.
Mvula alisema,hatua hiyo imesaidia makundi hayo hususan vijana nawanawake kupata mitaji iliyowawezesha kuanzisha shughuli za kujipatia kipato na hivyo kujikwamua na umaskini.