Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhji Hasani Kabeke, akizungumza na maelfu ya waumini wa Kiislamu waliofurika kuswali Sala ya Idd El Fitri, kwenye Uwanja wa Nyamagana, leo.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhji Hasani Kabeke, akiongoza maelfu ya waumini wa Kiislamu waliofurika kwenye Uwanja wa Nyamagana, kuswali Sala ya Idd El Fitri, leo.
Waumin wa Kiislamu, wakiswali Sala ya Idd El Fitri kimkoa, katika Uwanja wa Nyamagana, leo (Picha na Baltazar Mashaka)
………….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
Waislamu mkoani Mwanza wameaswa kudumisha amani, upendo na mshikamano katika jamii, huku wakihimizwa kuendeleza matendo mema waliyoyafanya katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Miongoni mwa matendo hayo ni pamoja na kulipa zaka na kuyajali makundi yenye uhitaji, hususan yatima, ili kuimarisha ustawi wa kijamii na mshikamano wa kitaifa.
Wito huo ulitolewa leo na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, baada ya Sala ya Idd El Fitri iliyofanyika kimkoa katika Uwanja wa Nyamagana, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa dini ya Kiislamu na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Alieleza kuwa bila kuwepo kwa amani, ibada haziwezi kufanyika ipasavyo na hata juhudi za maendeleo hushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa sababu ya vurugu, hivyo aliwasihi waislamu kuilinda na kuihubiri amani katika maisha yao ya kila siku, sambamba na kuheshimu viongozi wa dini na serikali.
“Amani ya kule tunakokwenda kuhiji imeharibika, twende kuiombea dunia amani iwe sehemu salama ya kuishi.Tuiombee Tanzania izidi kuwa kisiwa cha amani, tumwombee Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, maana yapo baadhi ya mataifa yanawaondoa madarakani viongozi wao,” alisema Sheikh Kabeke.
Aidha, aliwataka waumini kushikamana na kuepuka migawanyiko inayotokana na ukabila, ukanda, taasisi au mitazamo tofauti, akisisitiza umuhimu wa kujenga umoja wa kitaifa.
Kiongozi huyo wa kiroho alisema kuwa, ni vyema kwa waislamu kuishi kwa amani na watu wa imani za dini nyingine, akieleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani kinachopaswa kulindwa kwa vitendo.
Pia, aliwahimiza waumini kutekeleza wajibu wa kutoa zaka, akibainisha kuwa kama kuna jmbo litakalosababisha kuchomwa moto ni zaka iliyo nguzo muhimu ya Uislamu, akifafanua kuwa utoaji wa zaka unapaswa kuzingatia masharti yaliyowekwa, huku akionya kuwa, kushindwa kutoa zaka kwa wenye uwezo ni kinyume cha mafundisho ya dini.
Sheikh Kabeke akizungumzia vijana, alionya kuhusu mmomonyoko wa maadili, akibainisha kuwa baadhi yao wanajihusisha na vitendo visivyo na tija mitandaoni na kuiga mambo ya ovyo, badala ya kufanya kazi halali huku wakichagua aina ya kazi.
Alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali, zitakazowawezesha kusaidia dini yao, kujenga uchumi wao na taifa, huku Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omar Mtuwa, akiwataka waumini kusherehekea Idd El Fitri kwa amani, upendo, mshikamano na kuzingatia utu.