

Wafanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) wakipeana maelekezo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa laini maalum ya kusafirisha umeme kutoka Wilaya ya Masasi hadi Newala Mkoani Mtwara.
…………..
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kupitia Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), imetenga shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa laini maalum ya kusambaza umeme ya msongo wa kilovolti 33 kutoka Wilaya ya Masasi hadi Newala Mkoani Mtwara.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Abdallah Mitenda, amesema kuwa mradi huo wenye urefu wa kilomita 76 kutoka Masasi hadi Newala utasaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.
Mhandisi Mitenda amesema kuwa wakazi wa Masasi na Newala watanufaika na mradi huo kwa kufanikisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo kilimo cha korosho.
“Mradi huu unatumia nguzo za zege kutoka Masasi hadi Newala, na tutahakikisha unakamilika kwa wakati,” amesema Mhandisi Mitenda.
Meneja wa Mradi wa ETDCO, Mhandisi Charles Mashala, amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 68, huku akieleza kuwa kazi zilizofanyika hadi sasa ni pamoja na kusimamisha nguzo za zege 712 na kuendelea na utekelezaji wa kazi nyingine.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Abdul Mihambo, amesema kuwa utekelezaji wa laini hiyo unaendelea kwa kasi ili kufikia lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme katika Wilaya ya Newala.
Kwa upande wao, wakazi wa Wilaya ya
Newala wameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo, wakieleza kuwa utasaidia kukuza uchumi na kuwaletea maendeleo kwa ujumla.