SERIKALI YASISITIZA UWEKEZAJI MIUNDOMBINU NA USALAMA WA KIDIGITALI

Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki (Mb), amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ya TEHAMA ikiwemo minara, nyaya za mawasiliano, satelaiti na vituo vya data, ili kukuza sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari nchini.

Akizungumza Februari 26, 2026 katika kikao kazi kati ya Wizara na wadau wa Sekta Binafsi kilichofanyika katika viwanja vya Wizara, Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, amesema kuwa sambamba na uwekezaji huo, ni muhimu kuweka mkazo katika ulinzi na usalama wa kidigitali ili kulinda miundombinu dhidi ya vitisho vya kimtandao.

Aidha amebainisha kuwa hatua zinazotarajiwa kuhusiana na uanzishwaji wa akaunti ya Kidigitali ya Uchumi na Maendeleo ya Mkakati wa Uchumi wa Kidigitali zinatoa mwanga wa hatua za baadaye za utekelezaji, hivyo ni lazima kuweka kipaumbele katika utekelezaji wake kwa wakati.

Pia ameongeza kuwa Serikali inaendelea kujipanga kukamilisha na kutekeleza mpango kabambe wa Kitaifa wa TEHAMA kwa awamu, hususan katika maeneo yenye pengo kubwa la huduma, pamoja na kukuza uwekezaji wa sekta binafsi kwa kutoa motisha za kibiashara na kuhakikisha uwazi katika taratibu za upatikanaji wa ardhi na leseni.

Amesema kuwa hatua hizo zitasaidia kuimarisha usalama wa kidigitali kupitia sera, mafunzo na uwekezaji katika vituo vya ulinzi wa mtandao, pamoja na kuweka vigezo vya upatikanaji wa huduma kwa makundi dhaifu ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika uchumi wa kidigitali.

Kwa upande wake, Mchumi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango, Bw. Jordan Matonya, amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka ishirini na mitano imelenga kuongoza mabadiliko ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa mwelekeo wa sera na mipango yenye kulenga mwaka 2050.

Aidha amebainisha kuwa dira hiyo inalenga pia kuwaleta wadau pamoja ili kuimarisha ushirikiano katika sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari, hatua itakayotekelezwa kupitia mipango ya kitaifa ya kisekta na mipango ya kitaasisi kwa kipindi cha miaka ishirini na mitano ijayo.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Abdulla, amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kuendelea kuimarisha familia ya mawasiliano na teknolojia ya habari kwa kupanga na kutekeleza majukumu ya Taifa kwa pamoja, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 pamoja na sera na mikakati iliyopo ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani.

     

Post a Comment