NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini Fadhil Ngajilo ameungana na waumini wa dini mbalimbali katika kuadhimisha Sikukuu ya Pasaka kwa kutembelea wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, ikiwa ni jitihada za kuonesha upendo, mshikamano na faraja kwa jamii yake.
Katika ziara hiyo, Mbunge Ngajilo alipata fursa ya kuzungumza na wagonjwa pamoja na ndugu zao, akiwatia moyo na kuwatakia uponyaji wa haraka.
Alisisitiza kuwa kipindi cha ugonjwa ni changamoto kubwa kiakili na kimwili, hivyo ni jukumu la jamii kuendelea kuwapa faraja wale wanaokabiliwa na hali ngumu za kiafya.
Akiwa wodini, mbunge huyo alikabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo vyakula, vifaa vya usafi na bidhaa nyingine muhimu kwa baadhi ya wagonjwa. Alisema hatua hiyo ni sehemu ya kumuenzi Kristo kupitia matendo ya huruma yanayoakisi thamani ya Pasaka.
“Pasaka ni kipindi cha kutafakari na kukumbushana umuhimu wa upendo, huruma na kuwasaidia wanaohitaji. Wagonjwa ni sehemu ya jamii yetu, na wana haki ya kuhisi kuwa hatuwasahau,” alisema Ngajilo wakati wa kukabidhi msaada huo.
Kwa upande wao, baadhi ya wagonjwa na walezi wao walionesha furaha na shukrani kwa ujio wa mbunge huyo, wakieleza kuwa hatua hiyo imewapa faraja na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa. Walisema kitendo hicho ni mfano mzuri wa viongozi wanaogusa maisha ya wananchi wao moja kwa moja.
Ziara hiyo imepokelewa kwa namna chanya na wananchi wa Iringa, ambapo wengi wamesema ni hatua ya kuigwa na viongozi wengine, hasa wakati huu ambao jamii inahimizwa kujenga mshikamano na kuonesha utu katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka.
