HARABA: SERA YA UGAVI YA MWAKA 2025 ITAIMARISHA URATIBU NA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UMMA

Kaimu Kamishina wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Alex Haraba akizungumza na waandishi wa habari , akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha,, hawapo pichani, Jijini Dodoma, Aprili 4, 2026, kuelekea uzinduzi Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025, utakaofanyika Aprili 8, 2026.

Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog, Dodoma 

Kaimu Kamishina wa Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma katika Wizara ya Fedha, Alex Haraba, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha,amesema kuwa kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025 kunalenga kufungamanisha shughuli za Serikali ili kuimarisha uratibu na usimamizi jumuishi wa shughuli za mnyororo pamoja na kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya ugavi, kuboresha matumizi na usimamizi wa rasilimali za umma.

Aidha, amebainisha kuwa sehemu kubwa ya matumizi ya Serikali hupitia katika shughuli za ununuzi wa umma, na mnyororo wa ugavi ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa ufanisi, zinachochea ukuaji wa uchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Ameyabainisha hayo Aprili 4, 2026 jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025, Ambapo uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Aprili 8, 2026, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center Jijini Dodoma, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amebainisha kuwa katika shughuli za ununuzi wa umma, mnyororo wa ugavi ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa uwazi, ufanisi na uwajibikaji, ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Sera hii pia inahamasisha matumizi ya rasilimali na malighafi za ndani katika uzalishaji wa bidhaa na huduma, ili kuongeza thamani katika rasilimali za umma, kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani, makampuni ya ndani na kuimarisha ushindani wa uchumi wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Aidha, Sera hii inaweka mkazo katika utawala bora, matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa mnyororo wa ugavi, ushiriki wa sekta binafsi pamoja na kuimarisha ushiriki wa makundi maalumu ya kijamii, hatua inayolenga kupanua wigo wa fursa za kiuchumi na ajira kwa Watanzania.

Pia, amesema kuwa “Mwelekeo huu unaendana na maono ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi unaoongeza thamani katika rasilimali za ndani na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, biashara na maendeleo ya Taifa” Amesema Haraba

Aidha, ameongeza kuwa Kupitia utekelezaji wa Sera hii, Serikali inatarajia kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kupunguza upotevu wa rasilimali, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. ( Picha na Fullshangwe Blog )

Post a Comment