POLISI WAKANUSHA TAARIFA YA CHADEMA "HATUJAKAMATA MTU YEYOTE NKASI




Na mwandishi wetu

Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa leo Jumatano Januari 21, 2026 limekanusha taarifa zisizo sahihi zilizosambazwa mitandaoni zikidai kuwa Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA wamevamiwa, kukamatwa na kutawanywa kwa nguvu na Jeshi la Polisi wakati wakipanda Miti Wilayani Nkasi, Mkoani Rukwa.

Kupitia taarifa yake kwa Vyombo vya habari, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa amesema taarifa hizo za CHADEMA hazina ukweli wowote na zina lengo la kupotosha na kuzua taharuki zisizo na msingi kwani katika Wilaya ya Nkasi na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla hakuna tukio la matumizi ya mabavu ama la wafuasi wa Chama hicho kukamatwa na Jeshi la Polisi.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa linaendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao na tunaendelea kusisitiza wananchi kupuuza taarifa zinazoandaliwa na kusambazwa kwa lengo la kupotosha, kuchonganisha, kujenga chuki baina ya wananchi na Taasisi mbalimbali." Imesema taarifa hiyo ya Polisi.

Jana kupitia Mitandao ya Kijamii wafuasi mbalimbali wa Chadema akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. John Heche aliandika kupitia Mtandao wake wa X kuhusu taarifa hiyo potofu, akidai kuwa wafuasi wa Chama chake walivamiwa na kukamatwa kwa wale waliokuwa na mavazi ya Chadema wakati wa kupanda miti katika Ofisi za Chama hicho kama sehemu ya kuadhimisha miaka 33 tangu kuzaliwa kwa Chama hicho.

Post a Comment