WAKAZI WA MBAGALA KUTOKA KUGOMBEA DALADALA HADI KULA KIYOYOZI
WAKAZI WA MBAGALA KUTOKA KUGOMBEA DALADALA HADI KULA KIYOYOZI Na Mwandishi Wetu KUNA wakati safari ya kutoka Mbagala kwenda katikati ya Jiji la Dar es Salaam haikuwa tu suala la kufika unakokwenda, bali ilikuwa ni adha kubwa iliyokuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi. Kwa wakazi wa Mbagala na maeneo yanayounganisha ukanda huo na katikati ya jiji, usafiri wa kwenda kazini, sokoni, shuleni au kufanya biashara ulikuwa unahitaji uvumilivu mkubwa kutokana na msongamano, foleni na ushindani wa kupata nafasi kwenye daladala. Kwa akina mama wachuuzi wa samaki, adha hiyo ilikuwa na sura yake ya pekee. Kila siku walihitaji kusafiri kutoka Mbagala kuelekea Soko la Samaki Feri kununua samaki wa kuuza, wakiwa wamebeba ndoo zao na bidhaa nyingine. Safari yao haikuanza walipofika sokoni, bali ilianza tangu walipofika Mbagala Rangiratu kutafuta daladala ya kuwapeleka mjini, ambako walikabiliwa na changamoto ya kupata nafasi kwenye magari yaliyokuwa yamejaa abiria. Katika mazingira hayo, baadhi ya akina mama walijikuta wakilazimika kupandia kwenye madirish…