UMEME KUBADILISHA MAISHA YA WANANCHI VITONGOJINI
Serikali imedhamiria kubadilisha maisha ya wananchi vitongojini kupitia usambazaji wa umeme unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi wamehimizwa kuchangamkia kuunganishiwa umeme kwenye vitongoji vilivyofikiwa. Hayo yamesemwa Julai 15, 2026 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Mwamlula katika Kijiji cha Mseko na Kitongoji cha Kipeke katika Kijiji cha Masagi Wilaya ya Iramba Mkoani Singida. “Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameuwezesha Wakala wa Nishati Vijijini kuweza kutekeleza majukumu yake kisawasawa na anaendelea kuiwezesha ili kutimiza azma ya kuwafikishia maendeleo wananchi vijijini na vitongojini,” amesema Balozi Kingu. Amesema mpango uliopo ni kwamba ifikapo Mwaka 2030 vitongoji vyote 64,359 nchi nzima viwe vimefikiwa na umeme na kuwa hadi sasa asilimia 62.4 ya vitongoji tayari vimefiki…