TNCM YAIDHINISHA OMBI LA TANZANIA LA UFADHILI WA MZUNGUKO WA NANE (GC8) WA MFUKO WA DUNIA KWA KIPINDI CHA 2027–2029

TNCM YAIDHINISHA OMBI LA TANZANIA LA UFADHILI WA MZUNGUKO WA NANE (GC8) WA MFUKO WA DUNIA KWA KIPINDI CHA 2027–2029
Na. Mwandishi wetu - Dar es Salaam Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu na Kusimamia Fedha za Mfuko wa Dunia nchini Tanzania (Tanzania National Coordinating Mechanism – TNCM), imeidhinisha rasmi Ombi la Tanzania la Ufadhili wa Mzunguko wa Nane wa Mfuko wa Dunia (Global Fund Grant Cycle 8 – GC8) kiasi cha dola za Marekani milioni 538.6 kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu (TB) na Malaria, pamoja na kuimarisha Mifumo Thabiti na Endelevu ya Afya (RSSH), katika kipindi cha utekelezaji kuanzia Januari 2027 hadi Desemba 2029. Uidhinishaji huo umefanyika jijini Dar es Salaam katika kikao maalum cha TNCM kilichoongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa TNCM. Dkt. Yonazi amesema kuwa, mchakato wa maandalizi ya Ombi la GC8 ulianza rasmi tarehe 13 Machi, 2026 na umeendelea kwa zaidi ya miezi minne, ukihusisha mashauriano ya kina, majadiliano ya kitaifa, upangaji wa vipaumbele, uandishi wa andi…