BENKI KUU YAONGEZA RIBA HADI ASILIMIA 6.25 KUDHIBITI MFUMUKO WA BEI

BENKI KUU YAONGEZA RIBA HADI ASILIMIA 6.25 KUDHIBITI MFUMUKO WA BEI
Na John Bukuku Dar es Salaam Julai 3, 2026, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, ametangaza kuongezeka kwa Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 5.75 hadi asilimia 6.25 kwa robo mwaka unaoishia Septemba 2026, hatua inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei unaochochewa na kupanda kwa bei za mafuta, mbolea na gharama za usafirishaji duniani. Akizungumza Julai 3, 2026 katika makao makuu ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam, Gavana Tutuba alisema uamuzi huo ulifikiwa na Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) katika kikao chake kilichofanyika Julai 2, 2026, baada ya kutathmini mwenendo wa uchumi wa dunia na wa ndani. Alisema ongezeko hilo la riba linalenga kuhakikisha mfumuko wa bei unaendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5 huku ukiunga mkono ukuaji endelevu wa shughuli za uchumi nchini. Tutuba alisema pamoja na changamoto zinazosababishwa na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati, bei za chakula zinatarajiwa kupungua kutokana na mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa mwaka 2025/26. Aidh…